Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon ataka mapigano yasitishwe mara moja kaskazini mwa Mali

Ban Ki-moon ataka mapigano yasitishwe mara moja kaskazini mwa Mali

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametoa wito kwa pande zote kwenye mzozo nchini Mali kusitisha mapigano yao kaskazini mwa nchi bila kuchelewa.

Katika taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake, Bwana Ban amenukuliwa akieleza wasiwasi wake juu ya kukiuka kwa sitisho la mapigano nchini humo kwa kipindi cha siku chache zilizopita, huku utaratibu wa amani ukiwa unaendelea na makubaliano ya amani yakitarajiwa kusainiwa na pande zote za mzozo.

Taarifa zinasema tarehe 27, Aprili, vikundi vya waasi wa Touareg na Azawad, kutoka kwa jamii ya watu wanaohamahama walivamia mji wa Menaka, kwenye eneo la Gao na kupigana na kundi lingine la waasi wa Azawad.

Aidha tarehe 29, Aprili, kundi lingine tena la waasi wa Azawad limeshambulia makazi ya jeshi la kitaifa kwenye eneo la Timbuktu na kuua wanajeshi wawili na mtoto mmoja.

Wakati Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Mali, Bwaan Mongi Hamdi akijaribu kushawishi pande za mzozo kuendelea na mazungumzo, Katibu Mkuu Ban Ki-moon amezisihi kuonyesha msimamo wao katika utaratibu wa amani na kuheshimu makubaliano yao ya sitisho la mapigano la Mei, 23, 2014.