Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wahanga wa vita vya kemikali wakumbukwa, ikiwa ni miaka 100 tangu silaha hizo kutumika

Wahanga wa vita vya kemikali wakumbukwa, ikiwa ni miaka 100 tangu silaha hizo kutumika

Kumbukumbu ya mwaka huu ya wahanga wa vita vya silaha za kemikali ni ya muhimu saana kwani ni maadhimisho ya miaka 100 tangu kutumika kwa kiwango kikubwa kwa mara ya kwanza silaha za kemikali kwenye uwanja wa vita.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-moon kwenye ujumbe maalumu wa maadhimisho ya siku hii, akiongeza kwamba matukio ya Ypres ya mwaka 1915 ni lazima yawe kumbukumbu ya mbali lakini ukweli unaoogofya ni kwamba bado hivi sasa tunakabiliwa na athari zisizo za kibinadamu na zisizobagua za silaha za kemikali.

Amesema miaka 100 baada ya matumizi ya gesi ya Chlorine kama silaha ya vita huko Ypress, silaha hizo haramu bado ni tishio kwa maisha ya binadamu. Ban amesema inasikitisha kwamba miaka 90 baada ya mkataba wa Geneva wa 1925 na karibu miaka 20 baada ya kuanza kufanya kazi mkataba wa kupinga silaha za kemikali , orodha ya tunaowakumbuka siku hii inazidi kuwa ndefu.

Inaonyesha kwamba dunia imejifunza kidogo saana kutokana na yaliyotokea kale, akitolea mfano miaka miwli tuu iliyopita kumekuwa na ripoti za Syria kutumia silaha za kemikali zilizoushangaza ulimwengu na kuiamsha jumuiya ya kimataifa kwamba silaha hizo bado zipo na tishio kubwa kwa maisha ya binadamu.