Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban, OHCHR wasikitishwa na Indonesia kukatili maisha ya washtakiwa:

Ban, OHCHR wasikitishwa na Indonesia kukatili maisha ya washtakiwa:

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameeleza masikitiko yake makubwa kufuatia kitendo cha Indonesia kutekeleza adhabu ya kifo kwa watu waliopatikana na hatia dhidi ya madawa ya kulevya.

Ban amesema hatua hiyo ya Jumanne ni kinyume na wito wa kimaifa uliotaka serikali ya Indonesia kutotekeleza adhabu hiyo.

Taarifa ya msemaji wake imemnukuu hata hivyo akiendelea kuisihi Indonesia kutumia mamlaka yake kusitisha hukumu ya kifo.

Nayo ofisi ya Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR imesikitishwa na kitendo hicho ikisema ni kinyume na sheria za kimataifa.

Msemaji wa ofisi hiyo Rupert Colville amesema kwa mujibu wa sheria hizo adhabu ya kifo inapaswa kutolewa kwa wanaopatikana na hatia ya makosa makubwa kama vile kuua kwa kusudia lakini makosa yahusianayo na madawa hayako katika kifungu hicho.

Amesema haieleweki kabisa kwa nini Indonesia ambayo mara kwa mara husaka raia wake waliopatikana na hatia ugenini wasamehewe, ilikataa maombi ya kuonewa huruma kwa raia hao kwa kosa hilo ambalo si miongoni mwa makosa makubwa.

Bwana Colville amesema wamesikitishwa na kitendo cha raia hao kuondolewa uhai wao licha ya wito wa Katibu mkuu wa umoja wa Mataifa, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu na vyombo vingine wa kuitaka Indonesia kutotekeleza adhabu hiyo ya kifo.