Skip to main content

Kwenda sanjari na muda ni muhimu wasema UM ukiomba dola milioni 415 kwa ajili ya Nepal

Kwenda sanjari na muda ni muhimu wasema UM ukiomba dola milioni 415 kwa ajili ya Nepal

Ombi la dola milioni 415 limetolewa na Umoja wa mataifa kwa ajili ya waathirika wa tetemeko la ardhi nchini Nepal , huku hali ikielezwa kuwa mbaya na waathirika wengine bado hawajafikiwa.

Shirika la Umoja wa mataifa la kuratibu misaada ya kibinadamu na dharura OCHA limetoa ombi hilo na kusema kwenda sambamba na muda ni muhimu saana ikiwa sasa ni siku nne tangu kutokea kwa zahma hiyo.

Kwa mujibu wa OCHA moja ya vitu vya kuvipa kipaumbele ni ni kupanua wigo wa operesheni za misaada katika eneo lenye watu wengi la bonde la Kathmandu, baada ya watu Zaidi ya 5000 kupoteza maisha katika tetemeko hilo la wiki iliyopita.

OCHA, ambayo inaratibu juhudi za misaada za Umoja wa mataifa inasema kwamba wafanyakazi wa misaada wanapiga hatua poleole nje ya Kathmandi lakini changamoto za kiufundi bado ni kubwa.

Kwa miezi mitatu ijayo lengo ni kuwasaidia watu nusu milioni ambao wanasalia kuishi katika maeneo ya wazi kwa sababu nyumbazao zimeharibiwa au kubomolewa kabisa, na kupata msaada wa chakula kwa ajili ya watu milioni 1.4.

Watu takriban milioni 4.2 pia wanahitaji msaada wa haraka wa huduma za afya , madawa, chakula, maji ya kunywa na huduma za vyoo.