Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bongabongo yaanza Congo-Brazaville kulinda mazao ya porini Afrika

Bongabongo yaanza Congo-Brazaville kulinda mazao ya porini Afrika

Huko Brazaville, mji mkuu wa Jamhuri ya Congo, viongozi wa Afrika, wawakilishi wao na wataaamu wanakutana kwa siku nne kuandaa mpango wa kutokomeza biashara haramu ya mazao ya porini barani humo. Amina Hassan na maelezo zaidi.

(Taarifa ya Amina)

Mkutano  huo unasaka kupitisha mkakati wa kwanza wa aina yake wa kushughulkia biashara haramu ya wanyamapori na mazao ya porini wakati huu ambapo biashara hiyo inapotezea bara la Afrika mabilioni ya dola kila mwaka huku maliasili hiyo ikizidi kutoweka kwa kasi kubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la mazingira la Umoja wa Mataifa UNEP Achim Steiner amesema mkakati wa aina hiyo utokanao na waafrika wenyewe kwa kuzingatia mahitaji yao ni hatua muhimu sana katika kuondokana na biashara haramu ya kama vile magogo na wanyamapori.

Hata hivyo amesema pindi ukikamilika, utekelezaji wake utahitaji usaidizi thabiti wa kimataifa, mitandao kamili ya kubadilishana taarifa na sheria za uwajibishaji kwa wahusika bila kusahau elimu kwa umma juu ya umuhimu wake.

Paul Harrison, ni mshauri wa kimataifa wa usimamizi wa sheria wa shirika la mpango wa maendeleo la Umoja wa Mataifa.

(Sauti ya Paul)

“Tukiwa na mkakati huo, Afrika itakuwa na msingi ambao kwao nchi wanachama wake wanaweza kuanzia kuchukua hatua na tutaweza kuona mikakati zaidi ya kitaifa.”

Rasimu ya mkakati huo inatarajiwa kupitishwa kwenye mkutano wa wakuu wa muungano wa Afrika baadaye mwaka huu.