Skip to main content

Ban Ki-moon awaeleza wanafunzi wa Ufaransa matarajio yake kwa tabianchi

Ban Ki-moon awaeleza wanafunzi wa Ufaransa matarajio yake kwa tabianchi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ambaye yuko ziarani Ufaransa amesema vijana wana mchango mkubwa katika kufikia makubaliano juu ya mabadiliko ya tabianchi, wakati wa kongamano litakalofanyika mwezi disemba mjini Paris.

Amesema hayo akizungumza na wanafunzi wa chuo kikuu cha siasa cha Sciences Po mjini Paris, akieleza matumaini yake kwa kongamano hilo, na kusisistiza umuhimu kwa mataifa makubwa kushirikiana na kuafikiana juu ya tabianchi.

“ Mabadiliko ya tabianchi ni zaidi ya swala la mazingira, ni changamoto ya kiuchumi na ni swala la lazima kwa dunia. Wasiwasi wa kila siku kwa kila mtu unahusiana na mabadiliko ya tabianchi, iwe ni afya, usalama wa chakula, maji, hadi usalama wa kitaifa. “

Aidha amekariri wito wake kwa viongozi wa Ulaya kuongeza bidii ili kukabiliana na tatizo la usafirishaji haramu wa wahamiaji kwenye bahari ya Mediterenia.

Hatimaye amezungumzia tishio la ugaidi na msimamo mkali, akisema jamii ya kimataifa inapaswa kutokomeza uhalifu huo bila kulenga watu wa dini fulani dhidi ya wengine.