Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uuzaji holela wa antibayotiki moja ya sababu za usugu kwa tiba:WHO

Uuzaji holela wa antibayotiki moja ya sababu za usugu kwa tiba:WHO

Usugu wa dawa aina ya viuavijisumu au antibayotiki kwa magonjwa umesalia kuwa changamoto kubwa kwa nchi nyingi ulimwenguni na hivyo kukwamisha harakati dhidi ya magonjwa, imesema ripoti mpya ya shirika la afya duniani, WHO iliyotolewa leo.

Ripoti hiyo inafuatia utafiti ulioshirikisha serikali kwenye nchi 133 wanachama wa shirika hilo ambapo imebaini mambo makuu matano ikiwemo nchi 34 kati ya zilizoshiriki ndizo zenye mipango ya kitaifa ya kudhibiti usugu wa dawa hizo, uhaba wa maabara thabiti za kufuatilia usugu wa madawa na uuzuaji holela wa dawa hizo bila kibali cha daktari.

Halikadhalika ripoti imetaja suala la dawa zisizokidhi viwango, ukosefu wa miongozo ya matumizi yake na uelewa mdogo wa wananchi kuhusu athari za matumizi ya dawa hizo.

Dkt Charles Penn ni mratibu wa WHO kuhusu usugu wa antibayotiki.

“Bila hatua za haraka dunia inaelekea katika kipindi cha kutoweza kutumia kabisa antibayotiki ambapo magonjwa ya kawaida na majeraha madogo ambayo yamekuwa yanatibika kwa miongo kadhaa, saas yataweza kusababisha kifo na tutapoteza uwezo wa kutibu magonjwa makubwa kama vile uambukizo kwenye damu, numonia, kifua kikuu, Malaria na HIV.”

Nchi Nane kati ya 47 za Afrika ambazo zilishiriki utafiti huo zimesema usugu wa antibayotiki ni changamoto kubwa katika tiba dhidi ya Malaria na Kifua kikuu halikadhalika uduni wa ubora wa dawa hizo.