Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CERF yatoa dola milioni 15 kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Nepal

CERF yatoa dola milioni 15 kusaidia waathirika wa tetemeko la ardhi Nepal

Idadi ya vifo kufuatia tetemeko la ardhi la Jumamosi nchini Nepal inazidi kuongezeka pamoja na ya wale waliojeruhiwa pia katika nchi jirani. Nepal ambako inakadiriwa watu Zaidi ya 3300 wamepoteza maisha na Zaidi ya 6000 kujeruhiwa, idadi ambazo zinatarajiwa kuongezeka.

Watu milioni 8 katika wilaya 39 wameathirika huku milioni 2 wakiwa katika wilaya 11 zilizoathirika Zaidi.

Ili kukabiliana na athari zilizosababishwa na zahma hiyo mratibu wa misaada ya dharura Valarie Amos ametoa dola milioni 15 leo Jumanne kupitia mfuko wa dharura wa Umoja wa mataifa CERF ili kuwezesha mashirika ya misaada ya kibinadamu kuharakisha operesheni zake za huduma za haraka kwa watu wanaozihitaji nchini Nepal.

Kutolewa kwa fedha hizo kuna maanisha kazi ya kuokoa maisha ya watu itafanyika haraka na Bi Amos amewashukuru wahisani kwa kufanikisha fedha hizo.