Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa UNMISS akutana na watoto walioachiliwa huru na kikundi cha Cobra

Mkuu wa UNMISS akutana na watoto walioachiliwa huru na kikundi cha Cobra

Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, Ellen Margrethe Loej amesema kuachiliwa huru kwa watoto na vikundi vinavyowatumikisha vitani nchini humo kuende sambamba na kuwapatia huduma za msingi ikiwemo elimu, afya na ulinzi ili wasitumikishwe tena.

Amesema hayo alipotembelea mji wa Pibor leo Jumanne ambako pamoja na kukutana na watoto hao amekutana pia na David Yau Yau ambaye alikuwa kiongozi wa kikundi cha Cobra cha South Sudan Democratic Movement kilichokuwa kimetukimisha watoto hao.

Bi. Loej ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini, UNMISS amesema ametiwa moyo sana na mafanikio ambayo UNICEF na wadau wake wamepata katika kufanikisha kuachiwa huru watoto hao.

Hata hivyo amemsihi Bwana Yau Yau ambaye sasa ni mtawala mkuu wa eneo la Pibor asaidie kuachiliwa huru kwa watoto wengine 500 wanaoshukiwa kuendelea kutumikishwa na kikundi cha Cobra.

Mwaka huu pekee watoto 1,500 waliokuwa wakipigana sambamba kikundi cha Cobra wameshaachiwa huru ambapo zaidi ya 500 wameshaunganishwa na familia zao.