Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNCTAD yatoa mwongozo mpya juu ya marekebisho ya deni la Taifa

UNCTAD yatoa mwongozo mpya juu ya marekebisho ya deni la Taifa

Kamati ya maendeleo na biashara ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imetoa mwongozo utakaowezesha nchi kukabiliana na mzigo wa madeni kabla hali haijawa mbaya zaidi kama ilivyotokea huko Iceland, Argentina na Ugiriki kufuatia mdodororo wa kifedha duniani mwaka 2008.

Mwongozo huo uliochapishwa leo umeweka hatua ambazo nchi zinaweza kufuata kabla na wakati wa marekebisho ya deni la Taifa ambapo wataalamu wa UNCTAD wanasema mwongozo huo ni muhimu wakati huu ambapo sokomoko zaidi za madeni zinatarajiwa siku za usoni.

Misingi mitano kwa mujibu wa mwongozo huo wakati wa kufanyia marekebisho au kufuta deni la Taifa ni pamoja na uhalali wa deni, uwazi na kutokuwepo na upendeleo ambapo wadau wa ndani ya nchi wanatakiwa kushirikishwa kwa dhati pindi suala la ufutaji au mwendelezo wa deni linapojadiliwa.

Richard Kozul-Wright ambaye ni Mkurugenzi wa kitengo cha utandawazi na maendeleo cha UNCTAD amesema mzozo wa deni la Taifa unaweza kupatiwa suluhu mapema huku akisema kuchelewa kuchukua hatua mapema kunagharimu zaidi wadai na wadaiwa.

Zaidi ya wataalamu 20 wakwiemo wasomi wa sheria, wawekezaji, watunga sera na wawakilishi wa vyama vya kiraia walishiriki katika kuandaa mwongozo huo.