Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban Ki-moon afurahia amani kwenye uchaguzi Togo

Ban Ki-moon afurahia amani kwenye uchaguzi Togo

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amekaribisha kufanyika kwa uchaguzi wa rais kwa amani nchini Togo, tarehe 25 Aprili. Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na msemaji wake.

Wakati Togo ikisubiri matokeo ya mwisho ya uchaguzi huu, Katibu Mkuu anawashauri viongozi wa kisiasa na wadau wengine wa kijamii kuendelea kukuza hali hiyo ya amani iliyopatikana katika utaratibu wote wa uchaguzi.

Aidha amewasihi wagombea wote na wafuasi wao kutatua mgogoro wowote utakaoweza kutokea kwa kupitia njia za kisheria.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP umezisaidia mamlaka za serikali ya Togo katika maandalizi ya uchaguzi kupitia mradi wenye thamani ya dola 200,000.

Rais Faure Gnassingbe, ambaye ameongoza Togo tangu 2005 baada ya uongozi wa baba yake kwa miaka 38, anagombea awamu ya tatu katika uchaguzi huu.