Skip to main content

Ismail Ould Cheikh Ahmed wa Mauritania ateuliwa kuwa mjumbe maalum kwa Yemen

Ismail Ould Cheikh Ahmed wa Mauritania ateuliwa kuwa mjumbe maalum kwa Yemen

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ametangaza leo kumteua Ismail Ould Cheikh Ahmed kuwa Mjumbe maalum wake kwa Yemen. Katika jukumu lake bwana Ould Cheikh Ahmed atashirikiana na wanachama wa Baraza la Usalama, Baraza la ushirikiano wa ghuba,CGG , serikali za nchi wa Ukanda huo na wadau wengine, pamoja na timu ya Umoja wa Mataifa nchini Yemen.

Uteuzi huu unafuatia taarifa ya kujiuzulu kwa Jamal Benomar, ambaye Katibu Mkuu amemshukuru kwa juhudi zake zilizolenga kuwasaidia raia wa Yemen katika wakati wa mpito.

Kwa sasa Bwana Ould Cheikh Ahmed ni Mwakilishi Maalum wa Katibu mkuu na Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa kuhusu Ebola, UNMEER.

Aidha Katibu Mkuu Ban Ki-moon ametangaza leo kumteua Peter Jan Graaf kuwa Kaimu Mkuu wa UNMEER kuchukua kwa muda nafasi ya Bwana ould Cheikh Ahmed.