Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Malaria bado wasiwasi mkubwa kwa Afrika: Yvonne Chaka Chaka

Malaria bado wasiwasi mkubwa kwa Afrika: Yvonne Chaka Chaka

Leo ikiwa ni siku ya kimataifa ya kutokomeza malaria, Shirika la Afya duniani WHO limetoa wito kwa msimamo wa ngazi ya juu ili kufikia dunia isiyokuwa na malaria.

Katika taarifa iliyotolewa kwa ajili ya siku hiyo, WHO imesema kwamba bado malaria inaua zaidi ya watu 500,000 kila mwaka barani Afrika, wakati ugonjwa huu unaweza kuzuiliwa na kutibiwa.

Akihojiwa na redio ya Umoja wa Mataifa, Balozi Mwema wa Umoja wa Mataifa kwa ubia wa kutokomeza malaria, Roll Back Malaria, mwimbaji mashuhuri wa Afika Kusini

Yvonne Chaka Chaka amesema bado malaria ni wasiwasi mkubwa kwa bara la Afrika

“ Asilimia 80 ya visa vyote duniani na asilimia 90 ya vifo vinatokea barani Afrika kwa hiyo ni wasiwasi mkubwa kwa sisi. Na malaria ni moja ya sababu za kwanza za kutoroka shuleni. Watoto na hata walimu hawawezi kwenda shuleni, na hiyo ni shida kubwa”

Hata hivyo, mafanikio makubwa yamepatikana katika vita dhidi ya malaria, takwimu za WHO zikionyesha kwamba idadi ya vifo vyatokanavyo na malaria imepungua kwa asilimia 54 barani Afrika tangu 2000.

Kwa mantiki hiyo WHO inatarajia kuzindua mkakati mpya wa kutokomeza malaria kwa baada ya mwaka 2015, ambao utalenga kutokomeza malaria katika nchi 35 ifikapo mwaka 2035 na kupunguza kwa asilimia 90 visa vya malaria ifikapo 2030.

Halikadhalika mwongozo ulioboreshwa wa WHO kuhusu kuzuia malaria unasisitiza kutumia chandarua yenye viuatilifu, kupulizia dawa ndani ya nyumba, na wajawazito na watoto wadogo kukingwa dhidi ya Malaria na kumeza dawa sahihi ya Malaria.