Nina matumaini na makubaliano ya Fez: Dieng

24 Aprili 2015

Mkutano kuhusu dhima ya viongozi wa dini katika kuzuia uchochezi unaoweza kusababisha vitendo vya kikatili umemalizika huko Fez nchini Morocco kwa kukubaliana hatua za mpango wa utekelezaji zitakazojumuishwa kwenye azimio la Fez.

Akizungumza na Radio ya Umoja wa Mataifa mwishoni mwa mkutano huo, Adama Dieng ambaye ni Mshauri maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kuzuia mauaji ya kimbari amesema rasimu hiyo ya mpango wa utekelezaji ina vipengele vinane.

Amevitaja kuwa ni ufuatiliaji taarifa za kichochezi zinazoweza kusababisha uhalifu, kuanzisha kampeni dhidi ya kauli za kichochezi, kushirikisha katika mazungumzo wanaotoa kauli hizo na kuanzisha au kuangalia upya mfumo wa elimu na mitaala ya elimu ya watu wazima. Vingine ni.

(Sauti ya Dieng)

“Kuweka mijadala shirikishi kuhusu malalamiko ili kubaini chanzo chake ambacho mara nyingi husababisha ghasia kuibuka. Halafu pia kuimarisha uwazi wa fikra na utoaji ujumbe na hatimaye kushirikisha na kusaka kuungwa mkono na viongozi wa kisiasa.”

 Alipoulizwa iwapo ana matumaini na mwelekeo wa kilichokubaliwa Fez, Bwana Dieng amesema bila shaka kwa kuwa..

 (sauti ya Deng)

 “Niligundua kuwa viongozi wote wa dini waliokutana Fez walikubali na kuazimia kuwa hawataruhusu tena dini itumiwe vibaya hadi inachochea vitendo vya kihalifu.”

Rasimu hiyo ya mpango wa utekelezaji itajadiliwa katika mikutano mitano ya kikanda ya viongozi wa kidini itakayofanyika katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa na kwa mujibu wa Bwana Dieng, inatarajiwa kuridhiwa kwenye mjadala wa wazi wa viongozi hao mwezi Mei au Juni mwakani.

 

♦ Kurambaza ukurasa mahsusi wa Siku ya Kiswahili Duniani bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter