Skip to main content

Wavulana 282 na msichana mmoja waachiliwa na kundi la Sudan Kusini

Wavulana 282 na msichana mmoja waachiliwa na kundi la Sudan Kusini

Wavulana 282 na msichana mmoja wameachiliwa huru katika hatua ya mwisho ya kuwaachilia watoto waliokuwa wanahusishwa na kushikiliwa na kundi la watu wenye silaha la Cobra Sudan Kusini.

Kuachiliwa huko kumefanyika katika kijiji cha Labrab, kwenye jimbo la Jonglei. Hili ni kundi la mwisho la mlolongo wa kuachilia watoto ulioanza tangu Januari na kufuatia makubaliano ya Amani kati ya kundi la Cobra na serikali ya Sudan Kusini.

Kundi la Cobra lilijulisha shirika la Umoja wa Matyaifa la kuhudumia watoto UNICEF kuwa lina takribani watoto 3000 katika jeshi lake. Na kabla ya kuachiliwa UNICEF na mpango wa taifa wa tume ya upokonyaji silaha na kurejesha watu katika maisha ya kawaida wa Sudan Kusini NDDRC wamekuwa wakifanya mchakato wa kina wa uchunguzi wa kina na ukaguzi wa kila mtoto.

Jumla ya watoto ambao wamekwisha achiliwa na kundi la Cobra hadi sasa ni 1,757.