Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usambazaji wa chakula wakumbwa na changamoto Yemen: WFP

Usambazaji wa chakula wakumbwa na changamoto Yemen: WFP

Nchini Yemen, Shirika la Umoja wa Mataifa wa Mpango wa Chakula WFP linaendelea kusambaza chakula kwa zaidi ya watu 100,000 waliotafuta hifadhi katika maeneo ya mji wa Aden.

Msemaji wa WFP Elisabeth Byrs amesema hayo akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, akieleza kwamba WFP inakumbwa na changamoto katika usambazaji wa chakula kutokana na kuendelea kwa mapigano.

“ Ukosefu wa mafuta nchini humo unatusumbua na utaendelea kutusumbua kama tunataka kuendelea na kuongeza operesheni zetu endapo tutaweza kufikia maeneo yote. Ukosefu huo unazuia pia familia kupika chakula kama kawaida. Tunaona pia bei zinazidi kuongezeka na inaathiri familia maskini zaidi.”

Kwa mujibu wa WFP, ni watu milioni 12 nchini humo ambao wamekumbwa na ukosefu wa usalama wa chakula, idadi hiyo ikiwa imeongezeka kwa asilimia 13 tangu kuanza kwa mapigano.

WFP ilikuwa imepanga kusambaza msaada wa chakula kwa watu zaidi ya milioni 5 kabla mapigano hayajaibuka na tayari watoto 225,000 wamepokea biskuti za tende shuleni, na watu 76,000 wamepokea vocha za pesa ili kununua vyakula.