Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vifo vya raia vimeendelea kuongezeka Yemen katika siku chache zilizopita:UM

Vifo vya raia vimeendelea kuongezeka Yemen katika siku chache zilizopita:UM

Ofisi ya haki za binadamu ya Umoja wa mataifa imesema vifo vya raia vinaendelea kuongezeka nchini Yemen katika siku chache zilizopita. Tangu Machi 26 na April 22 idadi ya raia waliouawa ni 551 ikiwemo wanawake 31 na watoto 115 , huku wengine 185 wakijeruhiwa.

Pia majengo ya umma takribani 64 yameharibiwa au kusambaratishwa kabisa. Kwa mujibu wa msemaji wa ofisi ya haki za binadamu Rupert Colville tarehe 21 na 22 April pekee makombora mengi yameanguka katika maeneo ya jeshi na raia mjini Sana’a, Ibb, Hijja na Taiz na kusababisha vifo 40 na majeruhi Zaidi ya 100.

(SAUTI YA RUPERT COLVILLE)

“ Tarehe 21 April takribani raia 20 waliuawa na wengine 120 kujeruhiwa wakiwemo wanawake na watoto kutokana na makombora yaliyovurumishwa kwenye jengo la karibu na Faj Attan mjini Sana’a, makombora ambayo pia yaliharibu kiasi ofisi za Umoja wa mataifa, ikiwemo ofisi ya kamishina mkuu wa haki za binadamu nchini Yemen”