Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshikamano wa jamii ya kimataifa wahitajika kwa raia wa Syria: Angelina Jolie

Mshikamano wa jamii ya kimataifa wahitajika kwa raia wa Syria: Angelina Jolie

Mzozo unaoendelea Syria unazidi kuathiri mamilioni ya raia nchini humo pamoja na nchi jirani, wamesema wakuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu Misaada ya Kibindamanu OCHA, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi UNHCR na la Mpango wa Chakula duniani WFP pamoja na balozi mwema wa UNHCR Angelina Jolie. Taarifa zaidi na Priscilla Lecomte.

Mkuu wa OCHA Valerie Amos ameeleza kwamba bado usambazaji wa chakula unakumbwa na mapigano yanayoendelea nchini humo na kurushwa kwa makombora ovyo. Ameongeza kwamba hali ya raia wanaozingirwa kwenye baadhi ya maeneo kama kambi ya Yarmouk inazidi kuwa tete.

Aidha amewasihi wanachama wa Baraza la Usalama kufikia makubaliano ili kuchukua hatua kuhusu mzozo huo, ikiwemo kusitisha biashara ya silaha, kuanzisha uchunguzi kuhusu uhalifu unaofanywa kwenye maeneo yaliyozingirwa na kuanzisha kesi kwenye mahakama ya kimataifa ya uhalifu wa jinai.

Kwa upande wake balozi Maalum wa UNHCR Angelina Jolie amezungumzia athari za mzozo kwa wakimbizi milioni 4 waliokimbia Syria kwenda nchini jirani na wakimbizi wa ndani milioni 14 nchini Syria.

(Sauti Angelina )

"Takribani wakimbizi Milioni Nne wa Syria wameathirika na mzozo ambao hawahusiki nao, lakini bado wananyanyapaliwa,  na wanaangaliwa kama mzigo. Pande zinazopigana ndani ya Syria ndio zinawajibika kwa mzozo, lakini mzozo unazidi kuwa mbaya kwa sababu ya mvutano na ukosefu wa kuchukua uamuzi kutoka jamii ya kimataifa unaozuia Baraza la Usalama kutimiza wajibu wake."