Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuendelea kushikiliwa mahabusu waandishi habari wa Ethiopia hakukubaliki:UM

Kuendelea kushikiliwa mahabusu waandishi habari wa Ethiopia hakukubaliki:UM

Mwakilishi maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa maoni na kujieleza David Kaye,na mwakilishi maalumu wa Umoja wa mataifa kuhusu uhuru wa uwanachama na kukutana kwa amani Maina Kiai, leo wamesema kushikiliwa mahabusu kwa wanablogu sita wajulikanao kama “Zone Nine” na waandishi habari wengine watatu nchini Ethiopia tangu mwaka mmoja uliopita ni kitendo kisichokubalika.

Wanablogu hao waliotumia jukwaa la mtandao kuripoti kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa nchini Ethiopia walikamatwa April 25 na 26 mwaka jana na wamekuwa rumande tangu wakati huo.

Shirikisho la mahakama nchini Ethiopia limearifiwa kuwafungulia mashitaka chini ya sheria ya kupambana na tangazo la ugaidi ya mwaka 2009 , kwa kufanya kazi na mashirika ya nje ya haki za binadamu na kuchochea ghasia kupitia mitandao ya kijamii na kusaabisha kuyumba kwa nchi.

Kwa mujibu wa wataalamu hao kesi ya wanahabari hao imeahirishwa mara chungu nzima na kwamba kuendelea kuwashikilia ni jambo lisilokubalika na la kutia wasiwasi hasa wakati taifa hilo likijiandaa kufanya uchaguzi wa bunge Mai 24 mwaka huu.