Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Zahma Mediteranea, EU ilenge hatua za kudumu badala udharura: Zeid

Zahma Mediteranea, EU ilenge hatua za kudumu badala udharura: Zeid

Kamishna Mkuu wa haki za binadamu kwenye Umoja wa Mataifa Zeid Ra’ad Al Hussein amesema uamuzi wa jana wa viongozi wa Muungano wa Ulaya kuhusu udhibiti wa wahamiaji wanaovuka Mediteranea kusaka hifadhi barani humo hautakuwa suluhisho la zahma hiyo.

Taarifa ya ofisi ya haki za binadamu imemnukuu Kamisha Zeid akisema uamuzi huo unaojikita katika kuimarisha ulinzi kwenye mipaka na kudhibiti uhamiaji haujawahi kufanikiwa na hautaleta mafanikio yoyote hivi sasa kwani wasafirishaji haramu wa binadamu wanaibuka na mbinu mpya kila uchao.

Amesema suala la kuongeza mara tatu bajeti ya uokozi wa maisha ni jambo jema lakini amehoji mustakhbali wa wahamiaji watakaookolewa.

Kamishna Zeid ametaka nchi hizo za Ulaya ziachane na hatua za dharura na badala yake zijikite kwenye miradi ya kina inayoweka taratibu stahili za uhamiaji ambazo pamoja na mambo mengine zinakaribisha wale wanaohitaji hifadhi ya kimataifa.