Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Suala la kushambulia meli zilizobeba wahamiaji halina mashiko:Kutesa

Suala la kushambulia meli zilizobeba wahamiaji halina mashiko:Kutesa

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Sam Kutesa amepinga wazo la nchi za Muungano wa Ulaya la kutaka kushambulia kwa bomu meli zote zitakazokuwa zinavuka bahari ya Mediteranea zikiwa na wahamiaji na wakimbizi wanaokwenda kusaka  hifadhi barani humo.

Bwana Kutesa amesema hayo alipokuwa akijibu maswali ya waandishi wa habari katika mkutano wake alioitisha New York kutoa muhtasari wa mambo muhimu ambayo ameshiriki hivi karibuni.

(Sauti ya Kutesa-1)

Iwapo unataka kushambulia hizo meli, ni kabla hazijachukua abiria huko Libya. Lakini tatizo ni kwamba huko Libya hakuna upande ambao unaweza kushirikiana nao kukamilisha hilo kwani Libya inakaribia kuporomoka kabisa na iwapo hilo haliwezekani basi tatizo hilo litaendelea. Napinga kabisa wazo la kushambulia kwa bomu na kuharibu meli zilizobeba wahamiaji.”

Bwana Kutesa amesema anatambuwa kuwa Italia, Ugiriki na Malta ziko kwenye shinikizo la kupokea wahamiaji na wakimbizi hao lakini hilo ni suluhisho la muda mfupi kwa hiyo..

(Sauti ya Kutesa-2)

“Suluhisho la kudumu ni kuangalia chanzo cha uhamiaji huu. Baadhi yao ni ukosefu wa usalama kwenye baadhi ya nchi na kwingine ni umaskini. Ni lazima tushughulikia masuala hayo kwa kina na hivyo ndio tunaweza kutokomeza suala hili.”

Katika mkutano huo Kutesa alitaja mikutano kama ule wa stahamala uliomazilika hivi karibuni na mijadala kuelekea mkutano wa uchangishaji kwa ajili ya maendeleo utakaofanyika mwezi Julai mwaka huu huko Addis Ababa, Ethiopia.