Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Janga la Mediteranea, uamuzi wa EU uzingatia utu na haki za binadamu

Janga la Mediteranea, uamuzi wa EU uzingatia utu na haki za binadamu

Viongozi wa Muungano wa Ulaya, EU wameombwa kuweka mbele masuala ya utu, haki na uhai wa binadamu wakati huu wanapokutana kukubaliana hatua  za pamoja za kushughulikia janga la kibinadamu kwenye bahari ya Mediteranea ambako mamia ya watu wanazama wakielekea Ulaya kusaka maisha bora au kuokoa maisha yao. Taarifa kamili na Grece Kaneiya.

(Sauti ya Grece)

Wito huo umo kwenye tamko la pamoja la Kamishna Mkuu wa UNHCR António Guterres, Kamishna Mkuu wa haki za binadamu Zeid Ra’ad Al Hussein, mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu uhamiaji Peter Sutherland na Mkurugenzi Mkuu wa IOM William Lacy Swing.

Wamesema Muungano wa Ulaya umeundwa kwa misingi ya ubinadamu, mshikamano na kuheshimu haki za binadamu hivyo wanawaomba wakuu wa muungano huo wazingatia misingi hiyo na waonyeshe maadili na uongozi wa kisiasa wanapopitisha mpango wa utekelezaji wa kushughulikia janga hilo.

Kwa mantiki hiyo wamependekeza mambo matano ikiwemo kuanzisha mpango unaoongozwa na nchi hizo wa kutafuta na kuokoa wahamiaji bila kuchelewa wenye uwezo kama mpango wa awali Mare Nostrum.

Halikadhalika kuweka mazingira toshelezi na salama ya uhamiji ikiwemo kuruhusu wafanyakazi wa stadi za kati na fursa ya watu kuungana na familia zao na kuondoa ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wahamiaji na wakimbizi.