Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Dawa bandia bado kikwazo dhidi ya Malaria: WHO

Dawa bandia bado kikwazo dhidi ya Malaria: WHO

Kuelekea siku ya Malaria duniani tarehe 25 mwezi huu, Shirika la afya duniani, WHO wiki hii litatangaza miongozo iliyoboreshwa ya tiba dhidi ya Malaria ambayo pamoja na mambo mengine inajumuisha mapendekezo ya kinga ya ugonjwa huo dhidi ya wajawazito na watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

WHO inasema hatua hiyo ni muhimu ili kuondoa pengo kati ya tiba na kinga na kwa kuwa licha ya mafanikio yaliyopatikana kwenye kupunguza vifo vitokanavyo na Malaria bado watoto na wajawazito hususan barani Afrika hawapati tiba sahihi inayopendekezwa.

Mathalani WHO inataka uchunguzi wa kina ili tiba dhidi ya Malaria ipatiwe wale tu wenye Malaria na si vinginevyo na uimarishaji wa kinga dhidi ya Malaria kwa watoto na wajawazito, lengo likiwa ni kupunguza vifo vya asilimia 40 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 90 mwaka 2030.

Hata hivyo suala linalotia shaka kwenye vita dhidi ya Malaria ni dawa bandia ambapo watu Milioni 60 hawapati dawa sahihi dhidi ya Malaria kama anavyofafanua Peter Olumese, mtaalamu wa afya kutoka WHO.

“Kuhusu ubora wa dawa, suala la dawa bandia na zisizokidhi viwango bado ni tatizo kubwa na kwenye miongozo hii jambo muhimu ni kuhakikisha dawa ni za ubora na viwango vinavyotakiwa.”

Ujumbe wa siku ya Malaria duniani mwaka huu ni wekeza katika mustakhbali, tokomeza Malaria.