Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

MONUSCO iko tayari kuisaidia serikali ya DRC katika maandalizi ya uchaguzi

MONUSCO iko tayari kuisaidia serikali ya DRC katika maandalizi ya uchaguzi

Wakati maandalizi ya uchaguzi yakiendelea nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, na huku baadhi ya wawakilishi wa upinzani wakiwa wameomba mazungumzo ya kisiasa yafanyike kabla ya uchaguzi, msemaji wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, MONUSCO, Charles Bambara, amesema MONUSCO iko tayari kuratibu mazungumzo hayo, iwapo pande zote za kisiasa watakubali utaratibu huo.

Akizungumza leo na waandishi wa habari mjini Kinshasa, Bwana Bambara amesema MONUSCO imepewa jukumu la kusaidia serikali ya DRC katika maandalizi ya uchaguzi, kupitia azimio nambari 2211 la Baraza la Usalama.

Aidha msemaji huyo wa MONUSCO amemkariri Martin Kobler, mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini humo, akieleza kwamba mazungumzo hayo yanahitaji ushirikiano wa pande zote mbili.

Bwana Bambara ameongeza kwamba ni lazima upande wa upinzani na upande wa serikali wakubali utaratibu huo kabla MONUSCO haijaanza kuratibu mazungumzo hayo.

Hatimaye msemaji wa MONUSCO amekariri azimio la Baraza la Usalama likizisihi pande zote kuandaa mazingira yanayotakiwa ili utaratibu wa uchaguzi uwe huru, sawa, wenye amani, na sambamba na katiba ya DRC.