Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutesa awashukuru viongozi wa dini kwa ujasiri wao dhidi ya chuki

Kutesa awashukuru viongozi wa dini kwa ujasiri wao dhidi ya chuki

Sasa imetosha na mwelekeo wa ghasia unaoendelea hivi sasa ni lazima utokomezwe, amesema Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Sam Kutesa alipozungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa mjadala maalum kuhusu stahamala, mjadala uliokutanisha viongozi wa umoja huo na wale wa kidini kutoka sehemu mbali mbali duniani.

Bwana Kutesa amesema kuanzia Paris hadi Tunis, Garissa hadi Yarmouk, Johannesburg hadi Peshawar jamii zinagubikwa na ongezeko la ukosefu wa stahamala ambayo nyingine inachochewa kwa misingi ya dini.

Hivyo amesema viongozi wa dini wana dhima muhimu ya kuendeleza stahamala, maridhiano na jamii jumuishi na kwamba kinachotakiwa sasa ni kuwapatia ushirikiano ili waweze kueneza ujumbe wa amani, matumaini na makubaliano.

(Sauti ya Kutesa)

“Ni lazima tusongeshe kuheshimiana. Na kama ilivyoelezwa kwenye mkutano huu stahamala pekee haitoshi ni lazima tuzungumzie pia suala la kuheshimiana.”

Na ndipo akatoa shukrani zake kwa viongozi hao ambao pia walikuwepo kwenye mkutano huo na waandishi wa habari.

(Sauti ya Kutesa)

“Tunasema shukrani kwa Baraka zenu, shukrani kwa ushiriki wenu, shukrani kwa ujasiri wenu. Nawasihi, pazeni sauti kwa nguvu dhidi ya wale wanaochochea vitendo vya ghasia. Sasa imetosha.”