Hali Afghanistan bado ni tata: Šimonovic
Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu Haki za Binadamu, Ivan Šimonovic ambaye alikuwa ziarani nchini Afghanistan amesema hali nchini humo hivi sasa ni ya utata.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini New York baada ya kurejea kutoka Afghanistan siku ya Jumanne, Šimonovic amesema utata huo unatokana na kuimarika kwa mchakato wa amani sanjari na kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya raia.
(Sauti ya Simonovic)
“Tuna aina fulanai ya maandalizi ya mchakato wa amani na kwa upande mwingine mapigano yanaongezeka. Mwaka 2014 tulikuwa na kiwango cha juu cha vifo tangu mwaka 2009 tulipoanza kufuatilia. Wakati huo watu zaidi ya 10 waliuawa kila siku. Lakini mwaka 2015 umeanza vibaya watu zaidi ya saba wanauawa kila siku.”
Licha ya utata na mashambulizi yanayoendelea Bwana Simonovic amesema viongozi wa kijadi katika baadhi ya maeneo kama vile jimbo la Kapisa wameweza kuibuka na mbinu ya kuwawezesha kuendelea na maisha yao.
(sauti ya Simonovic)
Wazee wameweka mpango ambapo majeshi ya serikali yanadhibiti masoko hadi saa Tano asubuhi na baada ya hapo ni watalibani. Hivyo wafanyabiashara wanalipa sehemu ya ushuru wao kwa serikali wakati wa asubuhi na upande mwingine jioni.”
Akiwa ziarani, Msaidizi huyo wa Katibu Mkuu alikuwa na mazungumzo na viongozi mbali mbali wakiwemo wale wa Umoja wa kujihami wa nchi za magharibi, NATO ambao amesema wameahidi kuendeleza ushirikiano katika ulinzi wa raia ikiwemo kusaidia majeshi ya Afghanistan katika kuondoa mabomu yaliyotegwa ardhini.