Ban alaani chuki dhidi ya wageni Afrika Kusini
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amelaani wimbi la chuki dhidi ya wageni nchini Afrika Kusini ambalo limesababisha vifo vya watu saba katika majuma yaliyopita.
Taarifa iliyotolewa na msemaji wa Katibu Mkuu imesema Bwana Ban ametuma salamu za rambi rambi kwa familia za waathiriwa.
Katibu Mkuu amepongeza hatua na matamko ya Rais wa Afrika Kusini na serikali katika kushughulikia machafuko hayo.
Alipoulizwa katika mkutano na waandishi wa habari hii leo kuhusu alivyopokea machafuko nchini humo Ban amelezea anavyochukizwa na chuki dhidi ya wageni.
(SAUTI BAN)
"Ukatili dhidi ya wageni na jamii maskini, zilizotengwa na zilizoko katika mazingira hatarishi ni kinyume na maadili na havikubaliki."
Amekaribisha maandamano na matamko ya hadharani kutoka kwa raia wa nchi hiyo ya kutaka amani na utulivu dhidi ya raia wa kigeni.
Ametaka juhudi zifanyike kuepusha mashambulizi kama hayo katika siku zijazo na kusisitiza suluhisho la amani.