Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Viongozi wa kidini wana wajibu wa kukuza stahamala: Ban Ki-moon

Viongozi wa kidini wana wajibu wa kukuza stahamala: Ban Ki-moon

Leo mjadala maalum wa siku mbili kuhusu stahamala na maridhiano ukiendelea kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amewasihi viongozi wa kidini kukuza mawasiliano kati ya watu wa dini tofauti ili kupambana na mivutano na chuki. Taarifa zaidi na Flora Nducha.

(Taarifa ya Flora Nducha)

Akizungumza kwenye mkutano wa leo unaohusu umuhimu wa dini katika kujenga daraja la stahamala na maridhiano, Bwana Ban amesema maadili ya Umoja wa Mataifa ya kustahamiliana, kuvumiliana na kuheshimiana yanapingwa na vikundi vya magaidi na watu wenye msimamo mkali ambao wamesambaa duniani kote siku hizi.

Akisema ukatili hausababishwi na dini, lakini na watu, amewaomba viongozi wa dini washirikiane ili kupambana na chuki, ubaguzi au hisia dhidi ya watu wenye dini tofauti.

“ Makombora yanaweza kuua magaidi, lakini naamini kwamba utawala bora ndio utaua ugaidi. Ndio maana nawasihi kulaani ukiukaji wa haki zabinadamu na ukosefu wa usawa wa kisheria popote mtakapovishuhudia. Nawaomba pia kujitahidi kuipaza sauti ya watu walio wengi ambao wako na msimamo wa wastani, ili kunyamazisha wale wanaoubiri ghasia na chuki”