Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNCTAD yataja muarobaini wa utegemezi wa bidhaa moja kwa fedha za kigeni

UNCTAD yataja muarobaini wa utegemezi wa bidhaa moja kwa fedha za kigeni

Kamati ya maendeleo na biashara ya Umoja wa Mataifa, UNCTAD imetoa ripoti yake inayoweka bayana jinsi uchumi wa nchi zinazoendelea unavyozidi kuwa hatarini kutokana na utegemezi wake wa kuuza bidhaa nje ili kupata fedha za kigeni. Assumpta Massoi na ripoti kamili.

(Taarifa ya Assumpta)

Ripoti hiyo itokanayo na utafiti kwenye nchi 135 imesema theluthi mbili ya nchi hizo zinategemea malighafi kama vile mafuta, ngano, shaba ambapo bei zinapoongezeka kama ilivyokuwa muongo mmoja uliopita hakuna wasiwasi wowote lakini tatizo ni pale bei zinapoporomoka.

Kwa mujibu wa wachumi wa Umoja wa Mataifa waliohusika kwenye utafiti huo nusu ya nchi hizo ziko Afrika na tatizo siyo tu kwamba zinategemea bidhaa bali bidhaa hizo zinazotegemewa ni chache mno na Janvier Nkurunzinza ni mmoja wa waandishi wa ripoti hiyo kutoka UNCTAD.

(Sauti ya Nkurunzinza)

 “Kati ya mwaka 2010 na 2013 utegemezi wa kuuza bidhaa nje ili kupata fedha za kigeni uliongezeka. Hili si jambo zuri kwa sababu unakuwa mtegemezi kupindukia na iwapo lolote linatokea kwenye bidhaa husika uchumi wako unaathirika. Hii ni kwa sababu hicho ndicho chanzo pekee cha fedha za kigeni kutokana na mauzo ya bidhaa nje.”

Ili kukabiliana na hali hiyo UNCTAD inapendekeza nchi hizo kuongeza thamani katika bidhaa hizo badala ya kuziuza ghafi pekee mathalani mazao kama kahawa, korosho yasindikwe na kama ni pamba itengeneze bidhaa badala ya kuuza ghafi.