Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNDP yaanzisha mradi wa ajira za muda kwa ajili ya ukarabati wa Vanuatu

UNDP yaanzisha mradi wa ajira za muda kwa ajili ya ukarabati wa Vanuatu

Mwezi mmoja baada ya kimbunga PAM, nchi ya Vanuatu bado inahitaji msaada ili kuendeleza ukarabati wa muda mrefu, huku asilimia 90 ya mazao yakiwa yameharibika.

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo UNDP, limezindua mradi wa pamoja na mashirika mengine ya kimataifa ya kutengeneza ajira ya muda mfupi kwa ajili ya kuendelea na ukarabati na kuanzisha upya mfumo wa uchumi.

Kwa mujibu wa Sarah Bel, msemaji wa UNDP aliyezungumza leo na waandishi wa habari mjini Geneva, juhudi za serikali zimeanza na tayari mafanikio yanaonekana lakini bado bidii zinahitajika ili kurejesha huduma za afya, maji na vyakula na kuwapatia raia makazi kwenye visiwa vyote.

Ajira zitakazotengenezwa kupitia mradi wa UNDP zitalenga kuondoa uchafu uliojaa kwa sababu ya kimbunga PAM na ambao tayari unaathiri mazingira na afya ya wakazi wa visiwa hivi.