Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Israel- Palestina : Ban Ki-moon aeleza wasiwasi juu ya suluhu ya mataifa mawili

Israel- Palestina : Ban Ki-moon aeleza wasiwasi juu ya suluhu ya mataifa mawili

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ameisihi jamii ya kimataifa kujitahidi kurejesha tena Israel na Palestina kwenye meza ya mazungumzo, huku akieleza wasiwasi wake juu ya mwelekeo wa suluhu ya mataifa mawili.

Bwana Ban amesema hayo akizungumza kwenye mkutano wa leo wa Baraza la Usalama kuhusu Mashariki ya Kati uliojikita kwenye swala la Palestina.

«  Kwa kipindi cha miaka kadhaa tumeona bidii nyingi ili kufikia amani kutokana na suluhu ya mataifa mawili. Licha ya amani, kumekuwa miongo ya kukosa fursa na kushindwa ambayo imekuwa na gharama kubwa sana » 

Katibu Mkuu ameiomba serikali mpya ya Israel ikariri msimamo wake wa kuunga mkono suluhu ya mataifa mawili na  kuachana na operesheni za kujenga na kuhamishia raia wa Israel katika maeneo ya Palestina.

Kwa upande mwingine Bwana Ban amekaribisha makubaliano yaliyofikiwa baina ya Israel na Palestina ili kuirudishia serikali ya Palestina kiasi cha dola milioni 470 kutoka kwenye mapato ya ushuru uliokusanywa na Israel kwa niaba ya Palestina.

Hata hivyo, amesema bado ukarabati wa Gaza haujamalizika kutokana na vizuizi dhidi ya usafiri wa watu na vifaa vya ujenzi, ukosefu wa ufadhili na mivutano ya kisiasa.

Amesema ukosefu wa ufadhili kwa ajili ya wakimbizi wa ndani, na usaidizi wa vyakula, unaweza kuathiri usalama kwenye eneo hilo.