Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kushambulia watoa misaada ni kuwanyima wahitaji haki yao ya msingi: Amos

Kushambulia watoa misaada ni kuwanyima wahitaji haki yao ya msingi: Amos

Shambulio la kutisha la Jumatatu dhidi ya wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF huko Somalia ni kiashiria cha ongezeko la hatari zinazokumba watoa misaada kwenye mizozo.

Amesema Valerie Amos msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu misaada ya kibinadamu na mkuu wa ofisi ya usaidizi wa kibinadamu, OCHA kufuatia shambulio hilo lililosababisha vifo vya wafanyakazi wanne wa UNICEF.

Taarifa ya OCHA imemnukuu Bi. Amos akisema kuwa kulengwa kwa watoa misaada kunakwamisha uwezo wao wa kufikisha misaada kwa wahitaji na kwamba mashambulio dhidi yao kunaweza kuwa uhalifu wa kivita kwani ni ukiukwaji wa haki za kibinadamu na sheria za kimataifa.

Mkuu huyo wa OCHA ametaka wahusika wawajibike wakati huu ambapo idadi ya mashambulizi dhidi ya wafanyakazi hao inaongezeka kila mwaka.

Mathalani mwaka 2013 kulikuwepo na mashambulio 264 yakiathiri wafanyakazi wa misaada 474 akitanabaisha kuwa heshima kwa bendera ya Umoja wa Mataifa na ile ya shirika la msalaba na hilal nyekundi inatoweka kila uchao.