Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ukosefu wa usawa ni chanzo cha matatizo mengi duniani: Balozi Kamau

Ukosefu wa usawa ni chanzo cha matatizo mengi duniani: Balozi Kamau

Suala la ufadhili wa malengo ya maendeleo endelevu na njia za kutekeleza ajenda ya maendeleo ya baada ya mwaka 2015 ni mada ya mkutano maalum wa siku nne ulioanza leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani.

Akiongea wakati wa uzinduzi wa mkutano huo, Mwakilishi wa Kudumu wa Kenya kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Macharia Kamau, ambaye pia ni mmoja wa waratibu wa mjadala huo, amesema ana matumaini kwamba jamii ya kimataifa itapata njia za kutekeleza malengo 17 ya maendeleo ambayo yanatarajiwa kutangazwa na Umoja wa Mataifa , mwezi Septemba mwaka huu.

Balozi Kamau ameongeza kwamba matatizo yote yanayokumba dunia ya sasa yanasababishwa na changamoto tatu muhimu: umaskini, ukosefu wa usawa na uharibifu wa mazingira.

Ametolea mfano wa vifo 800 vilivyotokea kwenye bahari ya Mediteranea wiki hii akisema uhamiaji haramu unasababishwa na ukosefu wa usawa baina ya nchi za dunia.

Hata hivyo amesema ukosefu wa usawa unakumba raia ndani ya nchi zenyewe:

“ Naweza kuchukua mfano wa Kenya, ambapo ukosefu wa usawa ndani ya nchi yetu umekuwa moja ya changomoto zinazozidi kudhoofisha demokrasia yetu, usalama na amani kwenye nchi yetu yenyewe”.

Suala la ufadhili kwa ajili ya maendeleo litazungumzwa pia katika kongamano na kimataifa kuhusu uchangishaji fedha kwa ajili ya maendeleo litakalofanyika nchini Ethiopia mwezi wa Julai.