Hali mbaya ya kibinadamu kwenye kambi ya Yarmouk yalitia hofu baraza la usalama
Wajumbe wa baraza la usalama la Umoja wa mataifa wameelezea hofu yao kuhusu hali ya kibinadamu kwenye kambi ya wakimbizi ya Yarmouk nchini Syria.
Wajumbe hao wametoa wito wa fursa ya kufikisha misaada ya kibinadamu bila vipingamizi vyovyote kwenye kambi hiyo na pia kuwalinda raia wanaoishi kambini humo.
Wamekaribisha juhudi za UNRWA na naibu mwakilishi wa Umoja wa Mataifa za hivi karibuni nchini Syria na kusistiza haja ya kuunga mkono juhudi za misaada ya dharura kwa raia walioko Yarmouk ikiwemo kupitia ufadhili wa ombi la dola milioni 30 na kutoa msaada wa kidiplomasia na kisiaza kwa UNRWA.
Wajumbe wa baraza pia wameelezea umuhimu wa juhudi za Umoja wa Mataifa za kuwasaidia wakimbizi wa Kipalestina waliokwama kwenye kambi hiyo kwa kupitia mpango wa njia tatu ambazo ni kutoa msaada kwa wakimbizi ambao hawako tayari au wamekwama kambini hapo hawawezi kuondoka, kuwasaidia ambao wanataka kuondoka kwa muda, na mwisho kuwasaidia wakazi wa Yarmouk ambao tayari wameshakimbia.