Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mwakilishi wa UM Somalia alaani mashambulizi ya Garowe

Mwakilishi wa UM Somalia alaani mashambulizi ya Garowe

Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Somalia, Nicholas Kay, amelaani vikali mashambulizi dhidi ya gari la Umoja wa Mataifa yaliyotokea mjini Garowe na kusababisha vifo na majeruhi kadhaa.

Katika taarifa iliyotolewa leo na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo, UNSOM, Bwana Kay amenukuliwa akisema ameshtushwa sana na tukio hilo, na kusikitishwa sana na dharau ya magaidi dhidi ya maisha ya watu wanaofanya kazi kwa ajili ya mahitaji ya kibinadamu ya raia wa Somalia.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kinachodaiwa kuwa bomu la kienyeji limelenga gari la Umoja wa Mataifa, saa mbili za asubuhi, mjini Garowe, maeneo ya Puntland, nchini Somalia na operesheni za dharura zinaendelea.

Wenzetu wa Umoja wa Mataifa wamesikitika sana, amesema Bwana Kay, akiongeza kwamba Umoja wa Mataifa utaendelea kuwa karibu na raia wa Somalia.