Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ban asononeshwa na shambulio nchini Somalia

Ban asononeshwa na shambulio nchini Somalia

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki- moon ameelezea kusikitishwa kwake na shambulio la leo dhidi ya gari la Umoja wa Mataifa huko Garowe, eneo la Puntland nchini Somalia ambapo watu saba wakiwamo wafanyakazi wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF waliuwawa na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Taraifa ya msemaji wa Umoja wa Mataifa imemkariri Bwana Ban akituma salamu zake za rambirambi kwa familia na marafiki wa waathiriwa na kuwatakia waliojeruhiwa uponyaji wa haraka. Amelaani vikali shambulio hilo dhidi ya watu ambao wanafanya kazi za usaidizi wa kibinadmau na maendeleo kwa watu wa Somalia wakiwamo watoto wengi wao wakiwa na mahitaji makubwa.

Katibu Mkuu amesisitiza kuwa shambulio hilo halitazuia nia ya Umoja wa Mataifa ya kusaidia watu na serikali ya Somalia katika ujenzi mpya wa amani na mafanikio nchini humo.

Amewapongeza wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa wanotumika nchini Somalia na kusisitiza kuwa mashambulio ya uwoga kama hayo kamwe hayataweza kuuzuia umoja huo kuendelea kufany akazi kwa ajli ya amani ya nchi.