Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Šimonović alaani shambulio mjini Jalalabad

Šimonović alaani shambulio mjini Jalalabad

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu  Ivan Šimonović amelaani vikali shambulio lililosababisha vifo vya watu 35 na kujeruhi zaidi ya watu 100 mjini Jalalabad nchini Afghanistan wakiwamo watoto. Shambulio hilo limefanyika wakati Bwana Šimonović akiwa ziarani nchini humo.

Katika taarifa yake Bwana Šimonović amesema shambulio hilo limeambatana na milipuko mingine iliyokuwa imetegwa mjini.

Amesema muda mfupi baada ya shambulio hilo alikutana na gavana, ofisa wa polisi na mkuu wa majeshi na kuelezea rambirambi za kina za Umoja wa Mataifa kwa waathiriwa na familia zao na kuongeza kuwa sio tu analaani shambulio hilo bali pia nia ya kuwabagua raia wa Afghanistan na kusababisha mateso yasiyokubalika inayowakilishwa na shambulio hilo.

Akiwa mjini Jalalabad msaidizi huyo wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya haki za binadamu alikutana na maofisa wa serikali,wadau asasi za kiraia na vikundi vya wanawake.

Bwana  Šimonović ametaka waandaaji  na watekelzaji wa shambulio hilo kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Afghanistan hivi karibuni umetoa ripoti yake kuhusu mauaji ya raia ambapo vitendo hivyo vimeongezeka kwa asilimia 22 tangu mwak 2014 na viwango hivyo vimeendelea miezi ya mwanzo wa mwak 2015.