Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Usalama wa chakula sokoni Afrika ya Mashariki

Usalama wa chakula sokoni Afrika ya Mashariki

Kila mtu anahitaji chakula ili aweze kuishi. Hata hivyo mtu anaweza kuugua iwapo atakula chakula kilichoambukizwa  vijidudu, bakteria, kemikali au virusi. Kila mwaka, zaidi ya watu 350,000 hufariki dunia kwa sababu ya magonjwa yatokanayo na chakula, kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani WHO.

Kiasi kikubwa cha vifo hivyo kimesababishwa na bakteria aina za E-Coli na Salmonella zinazoleta madhara mbali mbali kuanzia kuharisha, hadi kuumwa homa ya matumbo, sumu kwenye damu na kifo.

Binadamu huambukizwa E-Coli au Salmonella kupitia chakula kilichooandaliwa bila kuzingatia safi, kilichochafuliwa na kinyesi, au nyama na samaki ambazo hazijapikwa vya kutosha.

Ikiadhimisha siku ya afya duniani mwezi huu wa April kwa kumulika usalama wa chakula kwa ajili ya afya ya binadamu na ukuaji wa uchumi, WHO imeeleza kwamba ni lazima kila mtu, kuanzia mkulima hadi mlaji kuzingatia masharti ya usafi wa chakula, na kujifunza jinsi ya kupika na kuhifadhi vyakula venye hatari ya kuambukizwa na vijidudu.

Je hali ikoje katika Ukanda wa Afrika Mashariki? Tuanzie mjini Mwanza, nchini Tanzania, ambapo Martin Nyoni wa radio Saut FM ametembelea soko la Tanganyika na kuzungumza na mama lishe.