Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ahadi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zitekelezwe: Ban

Ahadi za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi zitekelezwe: Ban

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema uongozi jasiri na ushirikiano wa dhati unahitajika miongoni mwa viongozi wa sekta ya umma na ile ya kibinafsi duniani wakati huu ambapo dunia itapitisha makubaliano mapya kuhusu mabadiliko ya tabianchi huko Paris.

Amesema hayo huko Washington DC wakati wa tukio kuhusu mabadiliko ya tabianchi lililoandaliwa ikiwa ni sehemu ya vikao vya Benki ya dunia na shirika la fedha duniani wakati wa msimu wa chipukizi.

Ban amesema uongozi jasiri na ushirikiano utawezesha kuwa na fungu la fedha ambalo litawezesha kushughulikia masuala ya kisiasa, kiuchumi na kisera.

Mathalani kisiasa yahitajika mwelekeo wa kuhamasisha dola Bilioni 100 kila mwaka ifikapo mwaka 2020 ambazo ziliahidiwa na nchi tajiri mwaka 2009.

Halikadhalika kiuchumi, kampuni zilitangaza dola Bilioni 200 mwezi Septemba mwaka jana hivyo sasa ni wakati wa kutekeleza ahadi ya kuwa na mifumo ya kupunguza utoaji wa gesi chafuzi.

Na jambo la tatu kwa mujibu wa Ban ni usaidizi wa kuweka sera zitakazowezesha kuweka viwango thabiti vya nishati isiyoharibu mazingira.

Katibu Mkuu amesema ataendelea kushawishi wadau wote ili mambo hayo matatu yaweze kujumuishwa wakati pamoja wakati wa mkutano wa mabadiliko ya tabianchi utakafoanyika Paris.