Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Idadi ya wanaokimbia machafuko ya kabla ya uchaguzi Burundi yaongezeka: UNHCR

Idadi ya wanaokimbia machafuko ya kabla ya uchaguzi Burundi yaongezeka: UNHCR

Ghasia na vitisho vinavyoambatana na maandalizi ya kabla ya uchaguzi nchini Burundi vimesababisha ongezeko la karibuni la watu kukimbia na kuomba hifadhi katika nchi za jirani za Rwanda, na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Zaidi ya raia wa Burundi 8000 wameomba ukimbizi katika nchi hizo jirani katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, ambapo Rwanda pekee maombi ni 7,099 na waliosalia wameomba Congo DRC. Raia hao wa Burundi ambao wengi wanatoka jimbo la Kirundo, zaidi ya asilimia 60 ni watoto na wengi wamewasili na vitu vichache sana.

UNHCR ikishirikiana na wizara ya Rwanda ya kukabili majanga na masuala ya wakimbizi, na wadau wengine wamekuwa wakitoa msaada kwa watu hao.

Raia wa Burundi wamekuwa wakiripoti kunyanyaswa na kutoweka kwa ndugu zao walio katika upande wa upinzani wa kisiasa.

Uchaguzi wa Rais, bunge , seneti na serikali za mitaa unatarajiwa kuanza mwezi Mei na kumalizika mwezi Julai mwaka huu.