Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vyombo vya usalama Burundi vizingatie ueledi: Ban

Vyombo vya usalama Burundi vizingatie ueledi: Ban

Harakati za Burundi za kuelekea uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu ni moja ya ajenda za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Alhamisi wakati huu ambapo Katibu Mkuu wa Umoja huo ametaka vyombo vya dola nchini humo kuzingatia ueledi vinapotenda kazi zake. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Baraza la usalama litafanya mashauriano kuhusu Burundi ambapo  Naibu Msaidizi wa Katibu Mkuu kuhusu masuala ya siasa Tayé-Brook Zerihoun atawapatia wajumbe muhtasari kuhusu maendeleo ya hivi karibuni wakati nchi hiyo ikijiandaa kwa uchaguzi wa Rais na wabunge kati ya mwezi Mei na Agosti mwaka huu na shaka na shuku kuhusu ukosefu wa utulivu.

Mashauriano hayo yanafanyika wakati tayari Katibu Mkuu Ban Ki-moon amekuwa na mazungumzo na Waziri wa Mambo ya ndani wa Burundi Edouard Nduwimana jijini New York ambapo walijadili matukio ya hivi karibuni kuelekea chaguzi hizo.

Bwana Ban ameelezea wasiwasi wake juu ya kuibuka kwa mvutano wa kisiasa nchini humo na kusihi warundi kusuluhisha tofauti zao za kisiasa kwa njia ya mashauriano badala ya ghasia.

Ametoa wito kwa serikali kuhakikisha vyombo vya usalama vinazingatia ueledi wakati vinavyoshughulikia tafrani zozote zile huku akisihi serikali ihakikishe pande zote za kisiasa zinaweza kushiriki kikamilifu, kwa huru na haki mchakato wa uchaguzi.

Katibu Mkuu amesema kwa kufanya hivyo, uchaguzi utakuwa halali zaidi na kupunguza mvutano.