Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mshauri wa UM kuhusu Yemen Jamal Benomar anajiuzulu:

Mshauri wa UM kuhusu Yemen Jamal Benomar anajiuzulu:

Jamal Benomar, mshauri maalumu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu Yemen ameelezea nia yake ya kuchukua majukumu mengine na kujiuzulu wadhia alionao sasa.

Mrithi wake atatangzwa hivi karibuni, na hadi wakati huo Umoja wa mataifa umesema utaendelea na juhudi za kuanza tena mchakato wa Amani ili kurejesha hali ya kipindi cha mpito cha kisiasa katika mstari unaotakiwa.

Bwana Benomar kwa miaka mine iliyopita amekuwa akifanya kazi kwa karibu na watu wa Yemen ili kuhakikisha nia yao na matakwa yao ya kuwa na mabadiliko ya kidemokrasia yanatimia.

Kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Benomar alisaidia kuafikiwa makubaliano ya  kipindi cha mpito hapo Novemeber 2011, alifanikisha kumalizika kwa mjadala wa kitaifa mwezi Januari 2014 uliochukua miezi 10, na pia alikuwa mpatanishi wa makubaliano ya Amani na ushirikiano wa kitaifa yaliyoafikiwa Septemba 2014.

Katibu Mkuu Ban Ki-moon amesema anashukuru kwa juhudi za bila kuchoka za Benomar kwa muda wote akichagiza muafaka na kuwa na imani na mustakhbali wa Yemen kwa njia ya amani.