Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP inagawa chakula Aden na kuonya kutowafikia wengi wanaohitaji msaada Yemen:

WFP inagawa chakula Aden na kuonya kutowafikia wengi wanaohitaji msaada Yemen:

Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) na washirika wake wanagawa chakula kwa wakimbizi wa ndani 105,000 mjini Aden Yemen kwa siku chache zijazo, lakini wanaonya kwamba kuna changamoto za kuwalisha mamilioni ya watu walio na uhaba wa chakula wakati usalama ukizidi kuzorota. Flora Nducha na taarifa kamili.

(Taarifa ya Flora)

Kwa mujibu wa Purnima Kashyap mwakilishi na mkurugenzi wa WFP Yemen shirika hilo limetoa wito kwa pande zote zinazohusika katika machafuko kuwaruhusu kuweza kugawa chakula na mafuta ili kuokoa maisha ya mmamilioni ya watu .

Wiki mbili za ongezeko la machafuko zimewaacha raia wengi wa Yemen bila chakula , wakiwa wamekwama katika miji na vijiji vyao na akiba ndogo ya chakula inazidi kuisha. Pia kuna upungufu mkubwa wa mafuta hususan aden na maeneo ya mji mkuu Sana’a.

WFP inasema hali hiyo inatia hofu hasa ukizingatia karibu nusu ya raia wote wa Yemen wanakabiliwa na uhaba wa chakula, wakihangaika kupanda au kununua chakula cha kutosha ili kuishi maisha bora.