Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Umoja wa Mataifa wapaswa kuzuia mizozo si kukabiliana nayo : Balozi Gasana

Umoja wa Mataifa wapaswa kuzuia mizozo si kukabiliana nayo : Balozi Gasana

Kuendeleza haki za kibinadamu kama njia bora ya kuzuia mauaji ya kimbari ni mada ya kitabu maalum kilichozinduliwa leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.

Kitabu hicho kilichochapishwa na taasisi ya Jacob Blaustein ya kuendeleza haki za binadamu kinaangazia aina za ukiukaji wa haki za binadamu ambao unaweza kusababisha mauaji ya kimbari na jinsi ya kuuzuia, kama mfano kulinda haki za uraia, dini au lugha kwa watu kutoka vikundi maalum ambavyo vinaweza kulengwa, na kupambana na ubaguzi, mateso, unyanyapaa na kila aina ya uhalifu dhidi yao.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Jan Eliasson, ameelezea wasiwasi wake juu ya mizozo inayoendelea siku hizi duniani kote ambapo baadhi ya watu wanalengwa kwa misingi ya kikabila au kidini.

Amezingatia umuhimu kwa Umoja wa Mataifa na watalaam wa maswala ya amani na usalama kuwa makini zaidi kuhusu dalili za mapema za uhalifu na ukiukaji wa haki za binadamu.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kudumu wa Rwanda kwenye Umoja wa Mataifa, Balozi Eugène-Richard Gasana amezingatia umuhimu wa kuchukua hatua mapema wakati dalili za ukiukaji wa haki za binadamu zikiwa dhahiri, akitaja mfano wa Rwanda ambapo mapema dalili hizo zilijulikana lakini, bado jamii ya kimataifa ikakosa utashi wa kutekeleza.

« Ni wajibu wa nchi wanachama na wajibu wa pamoja wa jamii ya kimataifa kuhakikisha kwamba dalili hizo za awali zinakabiliwa. Kila siku nilikuwa najaribu kuwaambia wenzangu wa Baraza la Usalama, kweli tumekaa hapa kukabiliana na mizozo au kuzuia mizozo ? »