Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Gari lalipuka kwenye lango la MINUSMA, laua na kujeruhi

Gari lalipuka kwenye lango la MINUSMA, laua na kujeruhi

Shambulio lililofanywa majira ya asubuhi huko Gao kaskazini mwa Mali limeua raia watatu na kujeruhi watu 16 wakiwemo walinda amani Tisa na raia Saba.

Kwa mujibu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, MINUSMA, majira ya saa Tano na nusu asubuhi kwa saa za Mali, gari moja lililokuwa linajaribu kuingia kwenye kambi ya Ansongo lililipuka kwenye lango kuu na kusababisha zahma hiyo.

Mwakilishi maalum wa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Mali, na mkuu wa MINUSMA Mongi Hamdi amesema walinda amani waliojeruhiwa ni kutoka Niger ambapo wawili kati yao hali zao si nzuri sana.

Ameelezea kushtushwa kwake na shambulio hilo dhidi ya walinda amani na raia wasio na hatia huku akilaani vikali.

Hata hivyoa amesema shambulio hilo halitakwamisha juhudi za MINUSMA za kurejesha amani na usalama nchini Mali.

Ametuma rambirambi kwa familia zilizopoteza ndugu na jamaa pamoja na serikali ya Mali huku akiwatakia ahueni ya haraka walinda amani na raia waliojeruhiwa.