Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kutokomeza ukatili wa kingono kwenye mizozo yawezekana: Bangura

Kutokomeza ukatili wa kingono kwenye mizozo yawezekana: Bangura

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na mjadala wa wazi kuhusu wanawake, amani na usalama duniani ambapo mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu kuhusu ukatili wa kingono kwenye mizozo amesema sasa dunia iko kwenye mwelekeo wa kukabiliana na vitendo hivyo. Taarifa zaidi na Assumpta Massoi.

(Taarifa ya Assumpta)

Bi. Zainab Hawa Bangura akinukuu ripoti ya Katibu Mkuu amewaeleza wajumbe wa baraza hilo kuwa matumaini yanatokana na pamoja na mambo mengine kuongezeka kwa ongezeko la mikataba ya amani kwenye mizozo inayozingatia harakati dhidi ya ukatili wa kingono.

(Sauti ya Bangura)

“Rasilimali nyingi zaidi zinaelekezwa kwenye mipango ya kudhibiti ukatili wa kingono na ukatili wa kijinsia kuliko awali, ingawa bado kuna pengo kulingana na changamoto. Hatimaye pia tunashuhudia uwajibika kwa uhalifu huu ambao kihistoria ulikuwa unapuuzwa. Hii inathibitishwa na kiwango kikubwa cha marekebisho ya sheria na uharamishaji wa ubakaji kwenye ngazi ya kitaifa.halikadhalika ongezeko la watuhumiwa kufunguliwa mashtaka kitaifa na kimataifa.”

Hata hivyo amesema safari bado ni ndefu hakuna kulegeza msimamo kwa kuwa ukatili wa kingono kwenye mizozo ni jambo ambalo limefumbiwa macho muda mrefu.