Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mkuu wa MINUSCA asema raia wa CAR bado wateseka na ghasia

Mkuu wa MINUSCA asema raia wa CAR bado wateseka na ghasia

Mkuu wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, MINUSCA, Babacar Gaye amewaeleza wanachama wa Baraza la Usalama kwamba licha ya mwelekeo bora katika maswala ya usalama na maridhiano, bado raia wa Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR wanaendelea kukuteseka na ghasia.

Akizungumza leo kwenye Baraza la Usalama, Bwana Gaye amesema ghasia hiyo imesababishwa na mvutano utokanao na msimu wa kuhamahama kwa wafugaji wa kabila la Fulani na pia waasi wa Anti-Balaka na wafuasi wa zamani wa kikundi cha Seleka kuendelea kupinga utawala wa sheria.

Mkuu huyo wa MINUSCA amesema bado baadhi ya jamii za waislamu ziko hatarini, licha ya juhudi za mashirika ya kimataifa. Aidha hali ya kibinadamu bado ni tete, huku idadi ya wakimbizi wa ndani ikiendelea kuongezeka.

Hata hivyo, Bwana Gaye amekaribisha mafanikio yaliyopatikana katika mazungumzo ya kisiasa kwa ngazi ya mitaani yaliofanyika mwezi Machi, ambayo yatakuwa msingi wa kongamano la kitaifa la Bangui linalotarajiwa kuanza tarehe 27, mwezi Aprili.

Kwa mujibu wa Bwana Gaye, kongamano la Bangui ni hatua muhimu katika utaratibu wa mpito wa CAR.

“ Ukamilishaji wa kongamano jumuishi la mazungumzo ya kitaifa ya Bangui ni hatua muhimu katika utaratibu wa mpito. Misimamo ya wadau wote wa kitaifa, wakiwemo viongozi wa siasa na vikundi vya waasi vyenye silaha ni muhimu ili kuendeleza utaratibu wa mpito na kufungua njia kwa hatua zijazo zikiwemo maandalizi ya uchaguzi na juhudi za maridhiano kwa muda mrefu”

Hatimaye ametoa wito kwa wadau wote wa kimataifa ili watimize ahadi zao kwa ajili ya mahitaji ya kibinadamu, wakati asilimia 13 ya mahitaji ya kibinadamu zimepewa ufadhili, akiongeza kwamba jamii ya kimataifa ina wajibu wa pamoja wa kuhakikisha CAR inarejelea kwenye njia ya amani na maridhiano.