Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uchunguzi ufanyike dhidi ya vifo vya raia Yemen:Zeid

Uchunguzi ufanyike dhidi ya vifo vya raia Yemen:Zeid

Kamishina mkuu wa haki za binadamu wa Umoja wa mataifa  Zeid Ra’ad Al Hussein, Jumanne amezikumbusha pande zote zilizo katika mgogoro wa Yemen kuhakikisha mashambulizi yanayosababisha vifo kwa raia yanachunguzwa na haki za binadamu na sheria za kimataifa za haki za binadamu zinaheshimiwa wakati wa mapigano.

Amesema mbali ya mamia ya wapiganaji pia maisha ya raia 364 yamepotea tangu Machi 26 mwaka huu, ikiwemo watoto 84 na wanawake 24. Huku raia wengine 681 au zaidi wakijeruhiwa , majengo ya umma zikiwemo hospitali , shule, viwanja vya ndege na misikiti ikisambaratishwa kabisa kutokana na mashambulio ya makombora na maroketi.

Ameongeza kuwa katika wiki iliyopita mashambulizi mitaani yameongezeka na hasa kwenye idadi kubwa ya watu kama eneo la Aden , kati ya makundi ya watu wenye silaha wanaomuunga mkono Rais Abdi Rabbo Mansour Hadi na wafuasi wa mkono Houthis na rais wa zamani Ali Abdullah Saleh Zeid amesisitiza kwamba pande kwenye mgogoro wa Yemen lazima zichukue hatua madhubuti kuepuka kuelekeza mashambulizi ya kijeshi katika maeneo ya raia na kuwa waangalifu kupita kiasi kuhakikisha maisha ya raia na mali zao vinalindwa dhidi ya hatari za operesheni za kijeshi.