Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Madhara ya biashara haramu ya wanyamapori ni zaidi ya mazingira: Kutesa

Madhara ya biashara haramu ya wanyamapori ni zaidi ya mazingira: Kutesa

Vitendo vya uhalifu wa wanyamapori na misitu vinakithiri na hivyo serikali na mashirika ya kiraia duniani kote yanapaswa kupatia umakini zaidi.

Hiyo ni kwa mujibu wa watoa mada kwenye kikao cha ngazi ya juu kilichofanyika Doha, Qatar Jumatatu ikiwa ni sehemu ya mkutano wa 13 dhidi ya uhalifu.

Miongoni mwa waliozungumza ni Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Sam Kutesa ambaye amesema uhalifu huo unashamiri kila uchao na kuwa chanzo cha fedha kwa mitandao ya wahalifu, ikienda sambamba na usafirishaji haramu wa binadamu, madawa ya kulevya na silaha.

(Sauti ya Kutesa)

"Madhara ya uhalifu utokanao na biashara haramu ya wanyapori na mazao ya misitu ni makubwa sana. Uhalifu huo ukiwa unajichotea mabilioni ya dola kila mwaka, unaharibu siyo tu mazingira bali ustawi wa kijamii na kiuchumi kwa jamii husika.”

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na udhibiti wa uhalifu na madawa ya kulevya, UNODC Yuri Fedetov amesema ofisi yake sasa inatafiti kiwango cha uhalifu huo duniani na ripoti itachapishwa mwishoni mwa mwaka huu na hivyo..

(Sauti yaYuri)

Ni matumaini yangu kuwa ripoti hiyo itatoa mtazamo dhahiri wa mtandao wa siri wa biashara hiyo na hivyo kusaidia kupunguza pengo kati ya utashi wa kisiasa wa kushughulikia suala hilo na hatua za kutokomeza uhalifu dhidi ya wanyamapori na mazao ya misitu.”

Takwimu zinaonyesha kuwa mwaka 2013 pekee tembo 20,000 na vifaru zaidi ya 1,000 waliuawa barani Afrika ilhali thamani ya biashara haramu ya bidhaa za mbao kutoka Asia Mashariki na Pasifiki ilifikia karibu dola bilioni 17.