Mazingira yanayochipusha ISIL yatokomezwe: Ban
Jamii ya kimataifa ni lazima ishughulikia mazingira yanayowezesha kikundi cha kigaidi kinachotaka kuunda dola la kiislamu, ISIL kushamiri.
Hiyo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon alipozungumza na waandishi wa habari mjini Doha,Qatar akisema ISIL au Da’esh ni moja ya changamoto kubwa zaidi zinazokabili ulimwengu kwa sasa.
Amesema ni kwa mantiki hiyo tarehe 21 na 22 kutakuwepo na mjadala wa ngazi ya juu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuhusu kustahimiliana na maridhiaono ambao pamoja na mambo mengine utaangazia suala hilo.
Kuhusu Yemen, Katibu Mkuu amesema mzozo huo wa ndani haupaswi kuachiwa uendelee kukua na hatimaye uwe wa kikanda.
“Nimekuwa nikipinga kwa dhati majaribio ya wahouthi kuchukua udhibiti wa nchi kwa nguvu. Hii haikubaliki. Lakini pia nina wasiwasi mkubwa juu ya ongezeko la operesheni za kijeshi. Idadi ya raia wahanga inaongezeka, miundombinu muhimu ya kijamii inaharibiwa. Nina Imani ya dhati kuwa mashauriano yanayoratibiwa na Umoja wa Mataifa ndio fursa bora zaidi ya kuzuia kushamiri zaidi kwa mzozo huo na naunga mkono kwa dhati jitihada za mjumbe wangu maalum Jamal Benomar.”
Kuhusu Iraq, Katibu Mkuu ametumia fursa hiyo kukaribisha kukombolewa kwa mji wa Tikrit. Hata hivyo amesema anatiwa hofu juu ya ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu na uharibifu unaofanywa na wanamgambo na vikosi vilivyo upande wa majeshi ya serikali.